Tiger Woods -Sikuwa nimelewa kwa kunywa pombe
Mcheza gofu maarufu duniani Tiger Woods, amesema hakuwa amekunywa pombe alipokamatwa akiendesha gari jimbo la Florida mapema hapo jana. Mchezaji huyo alifunguliwa mashtaka ya kuendesha gari akiwa amelewa, lakini amesema ulevi wake ulitokana na dawa alizokuwa amezinywa kwa ushauri wa daktari.

Polisi wa Palm Beach County,Forida, wamempiga picha akionekana kuwa mchovu na nywele zikiwa rafu.
“Nafahamu uzito wa kitendo nilichokifanya na nawajibika kikamilifu na vitendo vyangu,” alisema.Polisi walitoa picha ya Bw Woods, akionekana kutokuwa nadhifu, nywele zake zikiwa hazijachanwa na macho akiwa ameyatoa nje na kuonekana mwenye uchovu.
Alikamatwa katika mji wa Jupiter.
“Nataka umma ufahamu kwamba pombe haikuhusika kwa vyovyote vile. Kilichotokea ni madhara ambayo hayakutarajiwa ya kutumia dawa kwa ushauri wa daktari,” alisema.
“Sikugundua kwamba kuchanganya dawa kungeniathiri sana hivyo.”
Aliongeza, “Ningependa kuomba radhi kwa dhati familia yangu, marafiki na mashabiki. Nilitarajia nifanye vyema kuliko nilivyofanya.”
Stakabadhi za polisi zinaonesha mwanagofu huyo wa miaka 41 alisimamishwa na polisi nyakati za saa tisa alfajiri karibu na nyumbani kwake maeneo ya Jupiter na wakamzuilia.
Aliachiliwa huru kutoka gereza la Palm Beach County mida ya saa nne na nusu asubuhi.
Taarifa zinaonesha aliachiliwa huru “kwa kujitambua mwenyewe”, maana kwamba aliahidi kuandika kwamba atashirikiana katika shughuli za kisheria zitakazofuata.

Woods, hajashinda taji lolote kubwa duniani katika kipindi cha mwongo mmoja sasa
Akizungumzia afya yake hivi karibuni, alisema upasuaji ulimsaidia kuondoa maumivu makali mgongoni na kwamba hajawahi kujihisi vyema alivyojihisi baada ya upasuaji “katika kipindi cha miaka mingi.”
Maisha yake yalianza kuangaziwa sana mwaka 2009 alipo kamatwa na kushtakiwa kwa kutokuwa makini wakati akiendesha gari nje ya nyumba yake Florida.
Alikiri kuwa na uhusiano nje ya ndoa na kuomba radhi hadharani.
Alisema alipokea usaidizi wa wataalamu na kwamba angeendelea kupokea ushauri.
Kutokana na matatizo yaliyomsibu, alipoteza udhamini kutoka katika kampuni nyingi na akachukua likizo pia kutoka katika mchezo wa gofu kwa muda
Comments
Post a Comment