Serikali Yacharuka Suala la Maiti 7 Kuokotwa Mto Ruvu........Waziri Mkuu Atoa haya maagizo Mazito kwa Jeshi la Polisi
WAZIRI Mkuu,
Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi
la Polisi kufanya upelelezi kuwabaini waliohusika na mauaji ya watu
saba ambao miili yao iliokotwa pembezoni mwa mto Ruvu wilayani Bagamoyo,
mkoa wa Pwani, ikiwa kwenye mifuko ya sandarusi, ili hatua kali
zichukuliwe dhidi yao.
Waziri Mkuu
Majaliwa amesema serikali imepokea kwa huzuni kubwa taarifa ya kuokotwa
kwa miili hiyo Desemba 8, mwaka huu na kueleza kuwa matukio kama hayo,
likiwemo la mjasiriamali kuuawa baada ya kutekwa mkoani Tabora,
hayavumiliki wala kukubalika.
Alitoa maagizo
hayo jana katika Baraza la Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W)
lililofanyika kitaifa kijijini Shelui wilayani Iramba mkoani Singida.
Waziri Mkuu Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.
Alisema,
“Serikali kwa kushirikiana na Polisi, tena Waziri wa Mambo ya Ndani uko
hapa (akimzungumzia Mwigulu Nchemba aliyekuwepo katika baraza hilo),
tutaendelea na upelelezi ili wahusika wachukuliwe hatua kali.”
Jana akihojiwa
katika kituo cha televisheni cha Star TV, Mwigulu alisema uchunguzi
umebaini kuwa miili saba iliyookotwa Bagamoyo ni ya wahamiaji haramu.
Miili ya watu
sita ilikutwa Desemba 7, mwaka huu kando ya mto Ruvu wilayani Bagamoyo
ndani ya mifuko ya sandarusi na ikiwa imewekwa mawe ili isielee kisha
mifuko hiyo kushonwa kama mzigo wa mazao na kutupwa mtoni.
Mwili mwingine
uliokotwa Desemba 9, eneo hilo hilo na pamoja na kutokuwa katika mfuko
wa sarandusi, ulikuwa umevuliwa shati na kuonekana na majeraha mgongoni
na kwenye ubavu umekatwa na kitu chenye ncha kali.
Mwishoni mwa
wiki, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Boniventure Mushongi alisema
miili yote ilizikwa kwa kuwa ilikuwa vigumu kuwatambua kutokana na
kuharibika vibaya huku kukiwa hakuna kitambulisho chochote
kinachoashiria watu hao ni nani na wametoka wapi na kwamba Polisi
inaendelea na upelelezi kubaini waliohusika na mauaji hayo na
atakayebainika sheria itachukua mkondo wake.
Aidha, Waziri
Mkuu alisema serikali ipo macho kukabiliana na tishio lolote la usalama
na vyombo vya usalama vipo tayari muda na wakati wote.
Aliwataka
wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kutoa taarifa wanapoona kuna
hatari kwani viongozi wa dini na waumini wa dini hizo ndio walinzi wa
Taifa.
Alisema uwepo
wa vikundi vya uhalifu kama ‘panya road’ cha jijini Dar es Salaam ni
hatari kwa jamii, kwani vinadhuru na kuvuruga amani na kueleza kuwa ni
vijana na watoto wanaoishi katika jamii, walioko misikitini na
makanisani na kutaka waripotiwe katika vyombo vya usalama ili
washughulikiwe.
Alizungumzia
ugaidi na kubambikizwa kesi, na kusema serikali itaendelea kusimamia mtu
kupata haki zake na anayestahili adhabu, kuipata vile vile.
“Ni heri kuwa na watu 10 waliotoroka mahabusu kuliko mtu mmoja kukaa mahabusu kwa kesi ya kuonewa,” alisema Majaliwa.
Mwigulu anena kuhusu miili 7, Saanane
Akizungumza
jana kwa simu kuhusu vifo hivyo vya Bagamoyo, Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema serikali baada ya tukio hilo ilichukua
hatua kupitia vyombo vya usalama na tayari Mkuu wa Jeshi la Polisi
nchini, Inspekta Jenerali, Ernest Mangu amemhakikishia wanalifanyia
kazi.
“Kama
nilivyosema awali, hatujajua asilimia mia kwa mia kama watu hao
waliouawa wana connection (uhusiano) na wahamiaji haramu waliookotwa
wamechoka sana hivi karibuni (juzi).
“Kuna
wahamiaji 81 waliokotwa hawajitambui, wameishiwa nguvu kabisa, ni eneo
hilo hilo kulikookotwa miili hiyo, tumehisi watu waliowabeba wahamiaji
hao inawezekana wengine walikufa na kwa vile hawana utu, wakawafunga
katika viroba (sarandusi) na kuwatupa, Polisi wanachunguza hili kwa
kina,” alieleza Mwigulu.
Aidha, alisema pia Polisi inachunguza ikiwa miili hiyo ilitupwa kikatili na wasafirishaji wa binadamu ambao nao hawana utu.
Alipoulizwa kwa
nini wazikwe haraka bila vipimo vya vinasaba, Mwigulu alisema kuwa
alizungumza na IGP na kuelezwa kuwa miili hiyo ilikuwa katika hali mbaya
sana, lakini pia kuzikwa hakuzuii uchunguzi kufanyika kujua chanzo cha
vifo hivyo.
Kuhusu kupotea
katika mazingira ya kutatanisha Ofisa wa Ofisi ya Chadema, Makao Makuu
Dar es Salaam, Bernard Saanane Novemba 18, mwaka huu, Mwigulu alisema
aliona taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii na kwa kuwa alikuwa
akimfahamu, alimpigia simu na kubaini simu haipatikani.
“Nilishtuka
kuona hizi habari, binafsi ni rafiki yangu wa karibu, nilipoona hizi
habari nilimpigia na sikumpata, baada ya kuona simpati nilimpigia Mbowe
(Freeman- Mwenyekiti wa Chadema Taifa), lakini simu yake iliita kama
vile mtu yupo nje ya nchi,” alifafanua Mwigulu.
Hata hivyo,
alisema amemuagiza IGP awaagize polisi kumtafuta Saanane na kuhakikisha
ufumbuzi wa kupotea kwake unapatikana na kujulikana alipo.
Juzi,
Mwenyekiti wa Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania (UTG), Malisa
Godlisten akizungumza na waandishi wa habari, aliipa Chadema na taasisi
za umma zenye dhamana ya usalama wa raia saa 72 kuanzia jana kuhakikisha
Saanane anapatikana na kueleza umma chanzo cha vifo vya watu hao saba
ambao miili yao ilikutwa kando ya mto Ruvu, Bagamoyo.
Comments
Post a Comment