Balaa!maiti nyingine yazikwa, yafukuliwa

Maiti
ya Mariki Kimario juzi ilifukuliwa na baadaye kuzikwa upya sehemu
nyingine katika tukio jingine la kuchukua kimakosa maiti hospitalini.
Tukio
kama hilo lililotokea takribani wiki mbili zilizopita kwenye Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili (MNH), wakati ndugu walipochukua mwili kimakosa na
kwenda kuuzika Usangi mkoani Kilimanjaro kabla ya watu wengine kupewa
maiti ambayo si yao walipoifuata hospitalini hapo na kuibua tukio hilo.
Kutokana
na tukio hilo MNH ililazimika kulipa gharama za mazishi kwa familia
ambayo mwili wa ndugu yao ulizikwa na familia nyingine. Tukio hilo la
juzi lilitokea mkoani Arusha ambako Jeshi la Polisi lililazimika
kusimamia kufukuliwa kwa mwili huo kwenye Kijiji cha Elkisongo kilicho
Kata ya Kidinga wilayani Arumeru. Katika tukio hilo, ndugu walioenda
kuchukua maiti ya Leshai Ngoisaye, walipewa maiti ya Kimario na kwenda
kuizika takriban kilomita 50 kutoka Arusha mjini.
Miili
hiyo ilikuwa imehifadhiwa Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru. Wakizungumza
na Mwananchi jana, baadhi ya ndugu wa Kimario walisema tukio hilo
limesababishwa na kutokuwapo umakini kwa wafiwa na wahudumu wa chumba
cha kuhifadhi maiti. John Lesian, mmoja wa ndugu wa marehemu, alisema
walikwenda kuchukua mwili wa ndugu yao juzi, lakini walipofika
walionyeshwa mwili wa mtu mwingine.
Hali hiyo ilisababisha kuzuka kwa malumbano baina ya ndugu wa Kimario na wahudumu wa chumba hicho cha maiti.
“Maandalizi
yote ya kuchukua mwili na kwenda kuzika Rombo yalikuwa tayari,” alisema
ndugu mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jeremiah Shirima.
“Baada
ya hali hii ndugu walitoa taarifa polisi na ikajulikana mwili tayari
ulishachukuliwa na kuzikwa na hivyo waliomba kwenda kuufukua.”
Muhudumu
wa chumba cha kuhifadhi maiti wa hospitali hiyo, ambaye aliomba
kutotajwa jina, aliwalaumu ndugu wa marehemu kuwa hawakuwa makini.
“Mimi
si msemaji ila tukio limetokea na tayari mwili wa Kimario umefukuliwa
na kurejeshwa na mwili wa Leshai Ngoisaye umechukuliwa na kuzikwa,”
alisema
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Elkisongo alichokuwa anaishi Ngosaye, Lesiyoni Sikita
alisema tayari wamefanya mazishi mengine baada ya kuzika kimakosa mwili
wa Kimario.
Mkazi wa Kijiji cha Elkisongo, Samweli Ngalabali aliomba serikali kufanya tafiti kubaini sababu za kuongezeka kwa matukio hayo.
“Huu ni uzembe lazima serikali ichukuwe hatua,” alisema.
Comments
Post a Comment