UFAFANUZI WA SERIKALI KUHUSU UKOMO WA MADARAKA YA RAIS NA UHAI WA BARAZA LA MAWAZIRI

Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu ukomo wa madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwisho wa uhai wa Baraza la Mawaziri kwa kadri Tanzania inavyoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaofanyika Jumapili, Oktoba 25, mwaka huu, 2015.
Taarifa
iliyotolewa jana jioni, Jumatano, Oktoba 21, 2015, Ikulu, Dar es Salaam
na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Yohana Sefue imesema
kuwa Serikali imetoa ufafanuzi huo kuwasaidia wananchi kuelewa maelekezo
na matakwa ya Katiba na Sheria kuhusu ukomo wa madaraka ya Rais na
mwisho wa Baraza la Mawaziri kufuatia mijadala ya karibu katika vyombo
vya habari na mitandao ya kijamii.
Taarifa
hiyo imekariri Ibara ya 42(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inasema kuwa ukiacha sababu nyingine, mtu
anayechaguliwa kuwa Rais atashika madaraka ya kiti cha Urais hadi Rais
Mteule atakapoapishwa.
Ibara hiyo ya 42(3) inasema: ”Mtu
anayechaguliwa kuwa Rais, atashika kiti cha Rais hadi – (a) siku ambako
mtu anayemfuatia katika kushika kiti hicho atakula kiapo cha Rais.”
Taarifa hiyo imesema: “Hivyo,
kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais
anaendelea kuwa Rais, akiwa na madaraka na mamlaka yote na kamili
yanayoambatana na nafasi hiyo, hadi Rais Mteule anakapokula kiapo cha
Urais. Hivyo, ni vyema wananchi waelewe kuwa hakutatokea wakati wowote
ambapo hakuna Rais na Amiri Jeshi Mkuu mwenye mamlaka kamili na aliye
tayari kuyatekeleza mamlaka hayo. Lengo ni kuhakikisha kuwa haitokei
wakati wowote nchi yetu ikakosa Rais na Amiri Jeshi Mkuu.”
Imesisitiza taarifa hiyo: “Madaraka
na mamlaka ya Rais yapo, na hayapugui kwa namna yoyote ile, hata baada
ya Uchaguzi Mkuu, mpaka Rais Mteule atakapoapishwa.”
Kuhusu
ukomo wa Baraza la Mawaziri, taarifa imefafanua kuwa kwa mujibu wa
Ibara ya 57(2) ya Katiba, Waziri na Naibu Waziri ataendelea kushikilia
mamlaka ya nafasi yake hadi, ukiacha sababu nyingine, Rais mteule
atakapoapishwa.
Ibara hiyo 57(2) inatamka: “Kiti
cha Waziri au NaibuWaziri kitakuwa wazi litokeapo lolote kati ya mambo
yafuatayo – (f) Ukiwadia wakati wa Rais Mteule kushika madaraka ya Rais,
basi mara tu kabla ya Rais Mteule hajashika madaraka hayo.”
Taarifa
hiyo imeongeza kuwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wanaendelea kushikilia
nafasi zao, wakiwa na madaraka na mamlaka kamili yanayoambatana na
nyadhifa zao hadi mara tu kabla ya Rais Mteule hajashika madaraka.
Imemalizia taarifa hiyo: “
Naomba vyombo vya habari, vyenye jukumu la kuelimisha jamii,
kuwaelewesha Watanzania kuhusu utaratibu huu wakubadilishana madaraka
kati ya awamu moja ya uongozi wa nchi na nyingine. Madaraka na mamlaka
ya Rais yapo, na hayapungui kwa namna yoyote ile, hata baada ya uchaguzi
Mkuu mpaka Rais Mteule atakapoapishwa.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
Comments
Post a Comment