Mgawanyo wa kata wamtingisha Mbatia
James Mbatia
Wagombea
udiwani wa Chadema katika kata 16 za Jimbo la Vunjo lililopo mkoani
Kilimanjaro, wametangaza kutomuunga mkono mgombea ubunge wa jimbo hilo
wa NCCR Mageuzi ambacho ni kati ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), James Mbatia.
Madiwani
hao wametoa msimamo huo mbele ya Mwenyekiti wa Chadema Mkoa
Kilimanjaro, Phillemon Ndesamburo, baada ya jitihada za kuwatuliza
kugonga mwamba, hivyo kuongeza orodha ya maeneo ambayo vyama vya Ukawa
havijakubaliana hadi sasa.
Wakati
hali hiyo ikiendelea Vunjo, mgawanyo wa jimbo la Itilima mkoani Simiyu
baina ya Chadema na CUF umevunja mkutano wa uzinduzi wa kampeni za
mgombea ubunge wa Chadema uliokuwa uzinduliwe na Mke wa mgombea urais wa
chama hicho, Edward Lowassa, Regina Lowassa kama ilivyoripotiwa katika
ukurasa wa 31 wa gazeti hili.
Katika
tukio jingine mkutano wa mgombea mwenza wa Chadema, Juma Duni Haji
wilayani Nzega ulioripotiwa katika ukurasa wa 14 wa gazeti hili,
ulivurugwa baada ya wagombea wa CUF na Chadema kugongana.
Tukio la Vunjo
Kutokana
na mvutano uliopo, Ndesamburo alikutana na wagombea udiwani wa Chadema
kwa faragha jana asubuhi lakini taarifa zilieleza wako tayari kumfanyia
kampeni Lowassa lakini siyo Mbatia.
Ndesamburo
alipotafutwa na Mwananchi jana, alithibitisha kuwapo kwa hali hiyo na
kuongeza kuwa anamtafuta Mbatia ili kujadiliana na namna ya
kushughulikia suala hilo.
Mbatia
alipoulizwa, awali alisema aulizwe Meneja wake wa kampeni, Hemed
Msabaha, baadaye alisema,“Nilishasema kamati tendaji za jimbo za Chadema
na NCCR-Mageuzi zikae ziangalie vigezo vilivyosainiwa na makatibu wakuu
wa Ukawa na kama vitaonyesha Chadema ndiyo inastahili kusimamisha
madiwani kwenye kata zote 16 miye sina tatizo.”
Msabaha
alisema katika waraka wa makubaliano ya ndani ya Ukawa uliosainiwa
Agosti 13, mwaka huu, kulitolewa vigezo vitatu ambavyo ni matokeo ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, chama chenye diwani kipewe nafasi na chama
kilichofanya vizuri uchaguzi wa Serikali za mitaa 2014.
“Uchaguzi
wa Serikali za mitaa NCCR-Mageuzi tulifanya vizuri katika vitongoji na
vijiji vya kata 10 dhidi ya kata mbili za Chadema, Kwa hiyo kata 14
zilikuwa hazina mgogoro,” alisema.
Msabaha
alifafanua kuwa kwa kigezo hicho cha uchaguzi wa Serikali za mitaa
mwaka 2014, NCCR-Mageuzi ilipewa kata 10 na Chadema mbili lakini kukawa
na ubishani katika kata mbili. Hata hivyo, alisema baadaye Chadema
waligeuka na kwenda na agenda mpya kwamba vyama hivyo vigawane sawa kata
hizo
Wakizungumza
na waandishi wa habari wagombea hao walidai kuchukizwa na hatua ya
NCCR-Mageuzi kukiuka makubaliano ya kuachiana viti vya udiwani.

Comments
Post a Comment