Maalim seif amlipua Lipumba
Wafuasi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na pia
mwenyekiti mwenza wa muungano wa wapinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), Profesa Ibrahim Lipumba, wameanza kushughulikiwa na
kutakiwa kuchagua moja; kuendelea kuwa ndani ya chama hicho au kutoka.
Ingawa Profesa Lipumba alipojiuzulu uenyekiti, alisema ataendelea kuwa
mwanachama wa CUF, lakini Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif
Hamad amewataka wanachama waliokuwa wakimuunga mkono, kuamua moja,
kubaki ndani ya chama hicho kama alivyoamua mchumi huyo mashuhuri
duniani, au kutoka.
“Profesa Lipumba kajiuzulu CUF, wale waliojiunga CUF kwa sababu ya
Profesa, wanayo fursa ya kuamua kubaki CUF au kutoka,” alisema Hamad
juzi usiku.
Mbali na kuwataka wanaomuunga mkono Profesa Lipumba kuamua kutoka ndani
ya chama hicho au kubaki, wakati kiongozi wao akiwa ameweka wazi kuwa
hana nia ya kutoka katika chama hicho, Maalim Seif alitoa kauli zingine
kuashiria kutohitaji hata uanachama wa Lipumba ndani ya CUF.
“Kama ni treni inayokwenda Mwanza, ikifika Morogoro abiria watashuka,
lakini wengine watapanda, ikifika Kaliua watashuka abiria lakini wengine
watapanda,” alisema Maalim Seif alipofanya ziara ya ghafla katika Makao
Makuu ya CUF, Buguruni jijini Dar es Salaam juzi usiku.
Hamad amewahakikishia wanachama wa chama hicho waliokuwa wamezingira
ofisi hiyo, kuwa uamuzi wa Profesa Lipumba kujiuzulu wadhifa wake
hautausambaratisha Ukawa na CUF, ambayo kwa sasa haina Mwenyekiti wala
Makamu Mwenyekiti, lakini akasema imeendelea kubaki katika mikono
salama.
Alisema akiwa Katibu Mkuu na viongozi wenzake waliobaki, watahakikisha
kwamba chama hicho kinafikia malengo ya kuanzishwa kwake, ambayo ni
kuhakikisha kinakamata dola.
Alisema mwishoni mwa wiki hii, chama hicho kitaanza vikao vyake
kuzingatia hatua iliyotokea, ili wachukue uamuzi thabiti wa kukiongoza
chama hicho na kuhakikisha kinabaki katika mikono salama, hadi hapo
uchaguzi wa kumtafuta Mwenyekiti utakapofanyika.
Akizungumzia Ukawa, Hamad alisema baada ya hatua hiyo ya Profesa
Lipumba, alizungumza na viongozi wakuu wa umoja huo, akiwemo Freeman
Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema), James Mbatia (Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi)
na Emmanuel Makaidi (Mwenyekiti wa NLD) pamoja na mgombea urais wa
umoja huo, Edward Lowassa na wamehakikishiana kuwa hawatarudi nyuma.
“Tumehakikishiana kwamba Ukawa upo na umeimarika zaidi na hatutarudi
nyuma… Tumeona kwa namna unavyoungwa mkono na wananchi walio wengi,
Magufuli (mgombea urais wa CCM) Ikulu ya Magogoni hataiona,” alidai
Maalim Seif.

Comments
Post a Comment