Upinzani wambana Dk Migiro, AG bungeni

Waziri
wa Katiba na Sheria, Dk Asha Rose Migiro, jana alibanwa bungeni baada
ya wabunge wa upinzani kuhoji juu ya Muswada wa Sheria ya Kulinda Watoa
Taarifa za Uhalifu na Mashahidi wa mwaka 2015 wakieleza umewahishwa bila
sababu yoyote.
Dk
Migiro alikutana na kimbuga cha upinzani ikiwa ni siku moja baada ya
Bunge la 10 kuigomea Serikali ilipotaka kuingiza bungeni miswada mitatu
iliyohusu Wizara ya Nishati na Madini wakisema inahitaji muda mzuri.
Mapema
jana, Dk Migiro aliwasilisha ndani ya Bunge muswada huo akilitaka
lijadili na kuupitisha ili kutoa nafasi ya kuwalinda watu wa aina hiyo.
Akiwasilisha
maoni ya upinzani bungeni, msemaji wa kambi hiyo katika Wizara ya
Katiba na Sheria, Tundu Lissu alisema muswada huo hauna tija kwa muda
huo kwani unatoa nafasi finyu kwa wabunge kujadili jambo ambalo ni
muhimu zaidi kwa wananchi.
Lissu
ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema uharaka wa
muswada huo ni kiashiria tosha kwamba Serikali inataka kuminya uhuru wa
wabunge kupitia kwa kina sheria hiyo.
“Kanuni
zinasema kuwa, sheria inaweza kupitishwa kwa hati ya dharura ikiwa tu
kuna mambo ambayo yanataka kutokea ambayo ni pamoja na majanga au vita.
Je, kuna uharaka kiasi gani wa kupitisha muswada huu?” alihoji Lissu.
Mbunge
huyo mbali na kutoa ufafanuzi katika vifungu vingi katika muswada huo,
lakini alisisitiza kuwa ukipitishwa utakuwa umewanyima haki watu wa kada
ya chini na kuwapa mwanya viongozi wao.
Mbunge
wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alipinga vikali muswada huo pamoja na
namna ulivyowasilishwa na akazua mgogoro mkubwa baina yake na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG), George Masaju.
Malumbano
ya wawili hao yalianzia pale Mnyika aliposema kuwa Serikali ni dhaifu
katika suala zima la utungaji wa sheria jambo ambalo pia liliamsha
hasira za Spika.
Katika
hoja zake, Mnyika alipinga jinsi muswada ulivyokuwa ukitoa upenyo kwa
watu kutoa taarifa kwa wakubwa wao badala ya kuzipeleka kwa vyombo
vingine.
“Mfano,
muswada unaelekeza mtu kutoa taarifa kwa kiongozi wake yaani akiwa
mfanyakazi wa benki kuu anawezaje kutoa taarifa za ufisadi wa gavana kwa
gavana mwenyewe?” alihoji Mnyika.
AG
Masaju alipinga kauli za kuwa Serikali inafanya vitu dhaifu akisema
siyo nia yao, bali wanafanya kazi ya kupeleka miswada ili wabunge
wenyewe ndiyo wafanye uamuzi.
Kwa
upande wake, Spika Anne Makinda alimtaka Mnyika kuondoa kile
alichokiita ni upuuzi ili aweze kujadili mambo yaliyo mbele yake kwani
anaonekana kuwa hakuwa na maandalizi.
“Mnyika
mbona tunabishana sana kwa mambo ya kitoto, ondoa upuuzi wako sasa na
ujielekeze kwenye muswada wenyewe,” alisema Makinda.
Akichangia
hoja hiyo Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila
alipinga mfumo ambao unatumiwa katika kutengeneza sheria hiyo ya
kuwalinda watoa taarifa kwamba hauna maana yoyote.
Kafulila
alisema ndani ya Tanzania, kuna vitu vingi ambavyo vinafanywa ikiwamo
ufisadi mkubwa unaowahusisha watu wa ngazi ya juu lakini hakuna wa
kuwalinda.
“Mimi
nilipotoa taarifa humu ndani, kwanza Spika ulisema nilichokoza
mwenyewe, nikaenda kwa RCO (Ofisa Upelelezi) Mkoa wa Dodoma kisha kwa
IGP, lakini kote sikupata msaada wowote,” alisema Kafulila na kuongeza;
“Kutokana
na hilo, nikaamua kukimbilia Israel na kwenda kupiga magoti katika
ukuta wa Suleiman ili nipate ulinzi ambao hadi leo ndiyo nategemea.”
Kwa
upande wa wabunge wa CCM, Maria Hewa ndiye aliyekuwa mbunge pekee
ambaye alisema kuwa muswada huo ulikuwa na uharaka ambao haukutakiwa kwa
wakati huo.
Wabunge wengine wa chama hicho; Ismail Rage, Grace Puja na Dk Mary Mwanjelwa wote waliunga mkono muswada huo.
Mabishano
ya vifungu vya muswada huo yaliendelea huku Lissu akionekana kuwa mwiba
kwa Dk Migiro na AG lakini hata hivyo, vifungu alivyokuwa akivipinga
vilipitishwa kutokana na wabunge kuhojiwa na sauti za ndiyo kuzizidi
zile za hapana.
Hata hivyo, muswada huo haukupitishwa jana baada ya muda wa Bunge kuisha
Comments
Post a Comment