Simba yasajili jembe lililoivuruga Yanga
Wachezaji wa Gor Mahia
NI
Michael Olunga? Hapana! Simba imemuweka kwenye faili lake kiungo
mkabaji wa Gor Mahia, Aucho Khalid ambaye juzi Jumamosi aliivuruga Yanga
kwenye mechi ya ufunguzi ya Kombe la Kagame.
Habari
za uhakika kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa Aucho ana nafasi kubwa
ya kusajiliwa Msimbazi na tayari mazungumzo baina ya viongozi wa klabu
hizo yameanza ingawa viongozi wengine wa usajili wa Mnyama wameshauri
kwamba jina hilo lihifadhiwe, waangalie wachezaji wengine zaidi kwa vile
bado wana muda.
Straika
wa Gor Mahia, Olunga, ndiye aliyeifungia timu yake mabao yote katika
ushindi wa 2-1 kwenye mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar
es Salaam, bao la Yanga likiwa ni la kujifunga kwa mabeki wa Gor Mahia
katika harakati za kuokoa shuti lililopigwa na Donald Ngoma, ndipo beki
Dirkir Glay akajifunga.
Kutokana
na kasi ya Olunga na shida ya Simba ya kusaka straika katika kipindi
hiki cha usajili, wengi walidhani vigogo hao watashawishika na Olunga
lakini wao wamesema hapana ila anayezungumziwa kwao ni kiungo mkabaji
Aucho ambaye ni raia wa Uganda.
Hata
hivyo, Simba hawawezi kumng’oa Olunga kwani ana mkataba wa miaka minne
na timu yake ingawa inasemekana pia kuwa Wekundu hao wamevutiwa na
kiwango cha kipa wa Gor Mahia, Boniface Oluoch ambaye amewataka viongozi
wa Simba kwenda kuzungumza na viongozi wake.
Habari
kutoka ndani ya Simba, zinasema kuwa juzi Jumamosi wakati mechi hiyo
ikiendelea vigogo wa Simba walioongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya
Usajili, Zacharia Hans Poppe, walifuatilia mechi hiyo ingawa Olunga
alionyesha kiwango cha juu lakini hawana mpango naye kwani tayari
wamemnasa Laudit Mavugo.
Tayari
viongozi wa Simba walitamka kuwa watatumia michuano hiyo kupata
wachezaji wapya wenye sifa na kiwango cha juu kujaza nafasi za wachezaji
wa kigeni. Nafasi hizo ni za Emmanuel Okwi (aliyeuzwa Denmark) na
Raphael Kiongera (majeruhi).
Mpaka sasa inao wachezaji wanne wa kigeni; Hamisi Kiiza, Simon Sserunkuma, Juuko Murshid na Laudit Mavugo.

Comments
Post a Comment