chadema fomu za urais za moto
Wakati
leo saa 10 jioni ndiyo muda wa mwisho uliopangwa kurejesha fomu za
kuomba kuteuliwa kuwania urais ndani ya Chadema, hadi sasa hakuna
mwanachama hata mmoja aliyejitokeza kuzichukua.
Badala
yake zimetolewa kauli tofauti kuhusu kusuasua kwa mchakato wa kumpata
mgombea urais hadi chama hicho kulazimika kusogeza mbele tarehe ya
mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu.
Hali
hiyo inazidisha sintofahamu iliyougubika mchakato wa urais ndani ya
chama hicho na ndani ya Ukawa, kuwa huenda kuna ‘mtu wa nne’
anayesubiriwa kutoka nje ya chama hicho, kama ilivyoripotiwa na gazeti
hili, wiki iliyopita.
Likikariri
chanzo cha kuaminika ndani ya Ukawa, gazeti liliandika kuwa huenda
umoja huo na hasa Chadema, wanasubiri mgombea kutoka nje ya chama kwa
kuwa hata baada ya wajumbe wa vikao vya mashauriano kukubaliana kuwa
mgombea wa Ukawa awe Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, baadhi
ya wajumbe kutoka katika chama hicho wanadaiwa kukataa kutangazwa kwake.
Hata
baadaye walipoulizwa nini msimamo wao kuhusu tetesi za mpango wa
kumkaribisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutoka CCM, viongozi
na wabunge wa chama hicho walisema anakaribishwa mradi tu afuate kanuni
na taratibu.
Suala
la mgombea urais wa Chadema na Ukawa limeendelea kuteka mjadala wa
kisiasa nchini huku Watanzania wakisubiri kufahamu nani atateuliwa
kupambana na yule wa CCM, Dk John Magufuli, hali inayosababisha baadhi
ya watu kudai mchakato huo una mizengwe.
Hata
hivyo, Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa, Gaudence Mpangala
alisema anadhani hakuna mizengwe inayowazuia baadhi ya wanachama
wasiwanie nafasi hiyo kwa kuwa kanuni na taratibu za vyama ziko wazi.
Alisema anachokiona ni kwamba wanachama hawajajipanga kuwania nafasi
hiyo ya juu.
Kwa
upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk
Alexander Makulilo alisema wako watu ambao hawawezi kugombea nafasi ya
urais kuwakilisha vyama vyao kwa sababu wanawaogopa viongozi wa juu wa
vyama hivyo.
“Jambo
la msingi la kuangalia ni haki kutendeka katika kila mchakato katika
uteuzi lakini watu wanawania nafasi kulingana na walivyojipanga,”
alisema.
Alisema
wingi wa wagombea urais katika vyama si kigezo pekee cha kukua kwa
demokrasia bali mchakato wa kuwapata wagombea hao ukiendeshwa kwa haki
ndiyo demokrasia.
Alisema kuwa hakuna ubaya hata kama kuna mgombea mmoja anayewania urais bali kinachotakiwa kuangaliwa ni ubora wa mchakato.
Hakijaeleweka
Katika
mkutano wake uliofanyika mjini Mwanza Jumatano ambao ulipangwa kutumika
kumtangaza mgombea urais wa chama hicho, Mwenyekiti wa chama hicho,
Freeman Mbowe aliwaomba Watanzania wavumilie wakati wanakamilisha
taratibu za kumpata mgombea huyo.
Pia,
ilielezwa kuwa chama hicho kilikuwa kinasubiri mkutano wa Baraza Kuu la
Uongozi wa CUF unaofanyika leo, huku taarifa nyingine zikisema chama
hicho kilikuwa hakijampata mgombea mwenza kutoka Zanzibar.
Wakati
hayo yakiendelea, bado ratiba ya kuchukua fomu za urais na kurudisha
ilikuwa inaonyesha ni leo na hakukuwa na dalili zinazoonyesha watu
kujitokeza kuwania nafasi hiyo ya juu, ambayo mara kadhaa viongozi wa
chama hicho wametamka kuwa tayari wamempata mgombea anayefahamika ndani
na nje ya nchi.
Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Slaa aliliambia Mwananchi jana kuwa asingeweza
kusema lolote kuhusiana na suala hilo kwa sababu alikuwa nje ya ofisi.
“Wasiliana na watu walioko ofisini, wao wataweza kujibu vizuri swali lako,” alisema Dk Slaa.
Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Dk Slaa aligombea urais na kutoa upinzani mkali kwa mgombea wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
Gazeti
hili lilipotaka kufahamu iwapo safari hii Dk Slaa amechukua fomu,
alikataa kusema lolote akidai taarifa hizo zitapatikana kwa walioko
ofisini.
Wabadili ratiba
Akizungumzia
hali hiyo jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu
alisema kuna marekebisho yamefanyika katika tarehe hiyo ya mwisho
kurejesha fomu ambayo yatatangazwa ndani ya simu mbili au tatu ambayo
yalilenga kupisha mchakato wa kura za maoni.
“Unajua
viongozi wanatakiwa kusimamia kura za maoni majimboni, kwa hiyo tuliona
kwanza tumalize hili, suala la mgombea urais lisubiri kwanza.
Tunatarajia kutangaza tarehe mpya ya kurejesha fomu ndani ya siku
mbili,” alisema Mwalimu na kuthibitisha kuwa hadi wanasimamisha shughuli
hiyo hakukuwa na mwanachama yeyote aliyechukua fomu za kuomba kuteuliwa
kugombea urais.
Baadaye jioni jana, chama hicho kilitoa taarifa ya kusogeza mbele tarehe ya kurudisha fomu hadi Julai 31, 2015 saa 10 jioni.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, watiania wote watapaswa kurejesha fomu hizo
katika Ofisi ya Katibu Mkuu, Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni, Dar es
Salaam.
Taarifa
hiyo ilifafanua kuwa ratiba ya awali iliathiriwa na kitendo cha
kusogeza mbele tarehe za uchukuaji na urejeshaji wa fomu za ubunge baada
ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza majimbo mapya 26.
“Hatua
hiyo iliathiri ratiba ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania
uteuzi wa kugombea urais kupitia Chadema ambapo awali wanachama wenye
sifa walipaswa kuanza kuchukua fomu 20-25 Julai, mwaka huu,” ilisema
taarifa hiyo.
Mkutano Mbeya waahirishwa
Katika
hatua nyingine, ziara ya Dk Slaa aliyetarajiwa kuwasili na kuhutubia
mkutano jijini Mbeya leo imefutwa hadi itakapotangazwa tena.
Mratibu
wa chama hicho Kanda ya Nyasa (Chadema), Frank Mwaisumbe alisema sababu
ya kufutwa ni viongozi wa kitaifa kuendelea na vikao vya ngazi ya juu
jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti
wa Chadema mkoani hapa, Joseph China alisema ziara hiyo imefutwa
kutokana na viongozi wakuu wa kitaifa kutingwa na vikao vya Ukawa.
Viongozi wa kitaifa wa Chadema wakiwa Mwanza walitangaza kwamba wangefanya mikutano mingine, Mbeya, Arusha na Dar es Salaam.

Comments
Post a Comment