TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA KUHUSIANA NA MUSWADA WA MAHAKAMA YA KADHI
Sisii, Maaskofu
kutoka TEC, CCT na CPCT tumekutana leo tarehe Machi 30, 2015 hapa Dodoma ili kuomba kwa
pamoja juu ya mgawanyiko unaodhihirika wa dini za Kikristo na Kiislamu kutokana
na muswada wa Mahakama ya Kadhi. Maaskofu tuliokutana hapa hatuna hasira na
wala hatuongozwi na hasira wala mihemko katika kufikia maamuzi tunayofanya kama ambavyo wengine wanavyotutafsiri. Tunafikia maamuzi
yetu baada ya maombi na sala na tunasukumwa na upendo kwa wananchi ili kujenga
taifa lenye umoja, amani, utulivu na maelewano. Pia tumekuja kufuatilia kwa
kina Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya 2014 unaopendekeza, pamoja
na mambo mengine, marekebisho ya Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka
1964. Muswada huu unapendekeza kuanzishwa Mahakama ya Kadhi ambao utawasilishwa
Bungeni April 01, 2015 kwa hati ya dharura na hivyo kuufanya umma wa Watanzania
kutokujua maudhui yaliyomo katika muswada huo wakati bado hoja zetu za msingi tulizopeleka
kwenye Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge na kwa Waziri Mkuu hazijajibiwa.
Tangu tulipokutana Machi 10, 2015 ambako tulitoa tamko letu kuhusiana na
Mahakama ya Kadhi na Katiba Inayopendekezwa, tumekuwa tukiendelea kutafakari
juu ya yale tuliyokuwa tumesema katika matamko yetu mbalimbali na jinsi amani
na utulivu wa nchi yetu vinavyoendelea kumomonyoka siku zinavyokwenda. Kwanza tumeshangazwa na tabia ya viongozi wa serikali ya
kuitisha na kuendesha mikutano wanayodai ni ya viongozi wa dini lakini isiyo
rasmi. Machi 03, 2015 Waziri Mkuu aliitisha mkutano kupitia Mchungaji mmoja
ambapo hakuna hata kiongozi mmoja wa taasisi au Kanisa aliyeshiriki. Jambo la
kushangaza ni kile kilichotokea Machi 28, 2015 ambapo Mhe. Rais alishiriki
kikao cha kikundi ambacho sio rasmi yaani Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam. Tunasema
kamati hiyo siyo rasmi kwa sababu haina baraka za viongozi wa ngazi za juu wa
kidini wa Mkoa huo na haina mwongozo wa kazi zake. Mikutano ya jinsi hii kati
ya serikali na wale ambao imewaona kuwa ndio viongozi wa dini sio sahihi kwani
viongozi wa dini wana taratibu zao za kualikwa au kuwakilishwa katika mikutano
na viongozi wa serikali au wa dini au madhehebu mengine. Tunawashauri
wanaohutubia na wanaoshiriki mikutano hii wajue kwamba washiriki hawana uwezo
wa kuamua au kukubaliana na jambo lolote kwa niaba ya viongozi wao wa juu na
pia viongozi husika wa serikali wasifurahi kwamba ujumbe wao umewafikia
viongozi wa dini kwani hao washiriki sio wawakilishi rasmi na hawana uwezo wa
kutoa maamuzi au kukubaliana juu ya jambo fulani la kitaifa. Pili, tumekuwa
tukifuatilia kwa karibu juu ya muswada wa Mahakama ya Kadhi na tumebainisha
dhahiri kwamba kile tulichokuwa tunasema kitatokea kimeaanza kutokea bayana.
Yale yaliyotokea kwenye semina kuhusu Mahakama ya Kadhi kwa Waheshimiwa Wabunge
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 29, 2015 ambao ni wasomi, ni
ishara ndogo sana
ya kile kitakachotokea maeneo yote ya nchi yetu. SERIKALI KWA NIA MOJA NA KWA
SABABU TUSIZOZIJUA INAANZISHA VITA VYA KIDINI KATI YA WATANZANIA WAKRISTO NA
WAISLAMU. Tunashangazwa kuona jinsi serikali inavyonuia jambo hili ovu
litakaloleta balaa kwa nchi yetu wakati huu wa kuelekea kura ya Maoni ya Katiba
Inayopendekezwa na baadaye Uchaguzi Mkuu wa 2015. Kutokana na mambo hayo makuu
mawili hapo juu, sisi Maaskofu wa Jukwaa la Wakristo Tanzania
tunatamka kama ifuatavyo : Matamshi ya Mhe.
Rais akihutubia aliyowaita viongozi wa dini tarehe Machi 28, 2015 kuwa Mahakama
ya Kadhi ni ya Waislamu wenyewe na serikali haitajihusisha wala kugharamia
yanakinzana na kile kinachoendelea bungeni na nchini. Hapa tunajiuliza, endapo
maneno ya Rais ni kweli, mbona Bunge linaendelea kujadili kitu ambacho serikali
haitajihusisha wala kukigharimia ? Kwa mantiki hiyo, tunamtaka Mhe. Rais aagize
muswada huu uondolewe Bungeni na usijadiliwe tena kwa kuwa Utafiti wa Tume ya
kurekebisha sheria ulishaonyesha madhara ya uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi.
Vinginevyo, kuendelea kujadiliwa kwa muswada huu maana yake ni kwamba serikali
inajihusisha na itagharimia mahakama hiyo. Serikali ijue kuwa endapo Wabunge wa
dini za Kikristo na Kiislamu watapigana na kisha baadaye wananchi nao wakafanya
hivyo katika maeneo yao,
SERIKALI ITAKUWA NDIYO CHANZO CHA MAPIGANO HAYO. Kama
tulivyotamka hapo juu, kuhusiana na jambo hili tunamtaka Mhe. Rais aiepushe
nchi yetu na kuingizwa kwenye mapigano ya kidini ambayo kuyadhibiti itakuwa
vigumu sana (tafadhali rejea kinachoendelea huko
Nigeria).
Pia tunamwomba Mhe. Rais akumbuke na kutafakari kile kilichotokea na kinachotokea
nchi ya Afrika ya Kati kati ya kundi la Seleka (Waislam) na kundi la Anti
Balaka (Wakristo). Tunaamini kuwa viongozi wa serikali wanafahamu viongozi
rasmi wa dini na madhehebu ya dini. Kwa mantiki hiyo tunawashauri viongozi wa
serikali waache kabisa kutumia vikundi visivyo rasmi kualika mikutano
wanayodhani kuwa itakubalika na waumini wa dini hizo. Mikutano yote ya jinsi
hiyo itakayoitishwa ni batili na maamuzi yake hatuyatambui na hatutayatambua.
Bado Maaskofu tunasimamia Tamko letu la Machi 10, 2015 na tunawahimiza Wakristo
wajitokeze kwa wingi katika kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la wapiga
Kura na zaidi wajitokeze kwenda kupiga kura ya HAPANA wakati wa kura ya maoni
kwani Katiba inayopendekezwa ilifikia hapo kwa njia ya ubabe, ilikosa uadilifu
na mbaya zaidi ni RUSHWA YA AHADI YA MAHAKAMA YA KADHI ya iliyotolewa na Waziri
Mkuu kwa Waislamu wakati wa kupitisha Katiba Inayopendekezwa. Tunafanya hivyo
kwa dhamiri safi kwa sababu ya imani yetu na
kwamba sisi ni raia wa nchi hii na tuna haki ya kueleza mawazo yetu bila woga kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977
inavyotupa haki. Mwisho tunawaomba Wakristo wote waendelee kufunga na kuomba
kwa ajili ya utulivu na amani ya nchi yetu.
Comments
Post a Comment